Aneth, kiongozi wa kampuni ya madini, anakumbwa na masahibu yanayofuatana. Baada ya kubakwa na mtu wake wa karibu kibiashara, bado anajikuta kizimbani akikabiliwa na mashtaka mazito ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha. Hana kumbukumbu ya kuyatenda hayo, lakini ushahidi unamsulubisha hadharani.
Hayo yakiwa bado hayajapoa, ajali ya moto, ikihusisha basi la magereza na lori la mafuta inaua watu wengi. Aneth pia anadhaniwa kuwa amepoteza maisha lakini baadaye, uchunguzi wa polisi unagundua kuwa Aneth si miongoni wa waliohofiwa kufa.
Sakata linachukua sura mpya na kuwaleta pamoja waendesha mashtaka wawili, Dkt. Rehema Nsabi na Zeph Steven, mahasimu wa muda mrefu. Mmoja kati yao ana siri nzito moyoni, siri inayoyatesa maisha yake kwa zaidi ya robo karne, siri inayomfanya aajiri mpelelezi binafsi kufumbua fumbo hilo.
Kuhusu mwandishi
Philipo Oyaro alizaliwa Bunda, Tanzania. Ni mwalimu na mwandishi wa riwaya. Ana shahada ya Sanaa na Ualimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na amefundisha katika shule mbalimbali nchini. Kwa sasa, ni Mkuu wa Shule ya Mwasa Hope iliyopo mkoani Mwanza. Anajulikana kwa umahiri wake katika uandishi wa riwaya na maono katika fasihi ya Kitanzania. Miongoni mwa kazi zake ni Kiu ya Kisasi (2013), Risasi na Visasi (2020), na Mamluki (2023). Riwaya yake hii ya Dunia Duara ilishinda Tuzo ya Fasihi ya Kiswahili ya SAFAL-Cornell mwaka 2023.








Reviews
There are no reviews yet.