Kabula anazaliwa na kulelewa katika jamii inayotawaliwa na mfumodume. Anasimanzika kufukuzwa shule kwa sababu ya ujauzito huku aliyeshiriki naye ngono akiendelea na masomo hadi chuo kikuu. Wakati Kabula akiwa fukara mwenye jukumu la ulezi, mwenzake anakuwa Rais wa nchi asiyejali mtoto wake wa ujana. Katika hali isotarajiwa, Kabula anashuhudia mjukuu wake akifukuzwa shule kwa sababu ileile iliyomsibu yeye. Masikini Kabula wa watu. Alikubali kuishi chini ya mfumodume. Hata hivyo kwa mjukuu wake mambo ni tafauti kabisa! Yeye hakukubali. Kwani ameapa kupambana na mfumo huo; na hivi sasa yu’ njiani kuhakikisha Ujanajike na Ujanadume unakuwa daraja moja chini ya jua. Kwa hali ilivyo, ni dhairi mfumodume ni dubwana. Je! Mjukuu wa Kabula atalishinda? Twende sote hadi ukurasa wa mwisho.
Kuhusu Mwandishi
Dotto Rangimoto ni mziwanda wa Daudi Rangimoto na Rehema Chamchua. Amezaliwa na kukulia Morogoro Mjini. Elimu ya Msingi amepata Shule ya Msingi Chamwino na Elimu ya Sekondari ameipatia Shule ya Sekondari Morogoro. Rangimoto ni mtunzi wa mashairi, riwaya, hadithi fupi, hadithi za watoto na tamthilia.
Mwaka 2016 alishinda Tuzo ya Ushairi ya Meya wa Dar es salaam. Mwaka 2017 alikuwa miongoni mwa washairi kumi waliofanya vizuri kwenye Tuzo ya Ushairi ya Ebrahim Hussein. Mwaka 2017 kupitia diwani yake ya Mwanangu Rudi Nyumbani alishinda Tuzo ya Kiswahili ya Mabati-Cornell ya Fasihi ya Afrika ambayo hivi sasa yaitwa Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika. Mwaka 2020 alishika nafasi ya pili Tuzo ya Hadithi Fupi ya Kalahari. Mwaka 2022 alishinda Tuzo ya Kiswahili ya Safal-Cornell ya Fasihi ya Afrika kupitia riwaya hii ya UjanaJike. Kwa kushinda tena Tuzo ya Safal-Cornell kumemfanya aweke rekodi; kwani Rangimoto ni mtu wa kwanza na wa pekee kushinda tuzo hiyo mara mbili kwenye vipengele tafauti.
Reviews
There are no reviews yet.