Kitabu hiki, ni historia fupi ya John Mhina Sepeku ambaye alikuwa Askofu wa kwanza wa Kanisa Anglikana, Dayosisi ya Dar es Salaam, na pia Askofu Mkuu wa kwanza wa Kanisa Anglikana Tanzania. Historia hii imetegemea sana maelezo kutoka kwa watu mbalimbali waliomjua katika uhai wake. Mambo mengine yamemepatikana katika kumbukumbu nyingi zikiwemo za nyaraka mbalimbali.
Ni miaka Zaidi ya mia moja tokea kuzaliwa kwa Askofu Mkuu Sepeku na miaka arobaini na tatu tokea afariki dunia. Hivyo, ilibidi kuchukua tahadhari kubwa katika kuyapima hayo maelezo kwani baadhi yake ni ya watu ambao nao pia walielezwa na wengine.
Ingawa makusudio ni historia ya Askofu Mkuu Sepeku, lakini imekuwa pia historia fupi ya Kanisa Anglikana Tanzania, baadhi ya shule zake na vyuo vyake, na watu wengine wa kikanisa.
Ni matumaini yangu kuwa wewe msomaji utabarikiwa sana na historia hii fupi na kwa upande wa viongozi wa Kanisa kujaribu kufuata nyao za waliowatangulia kama Askofu Mkuu Sepeku.
Kuhusu Mwandishi
Jaji Ramadhani, mtunzi wa kitabu hiki ni mzaliwa wa Kiungani, Unguja Zanzibar. Baada ya kuhitimu Chuo Kikuu, Dar Es Salaam, nakupata shahada ya sheria, alijiunga moja kwa moja na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. Wakati huo huo alikuwa Katibu wa Halmashauri ya Mtaa wa Mtakatifu Albano wakati John Sepeku akiwa Askofu wa Dayosisi ya Dar es Salaam na hatimaye akiwa pia Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania.
Jaji Ramadhani ameshika nyadhifa kadha wa kadha hapa nchini na hata kimataifa. Alikuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar tokea mwaka 1980 hadi 1989, akawa Jaji wa Rufaa toka mwaka 1989 hadi Julai, 2010 na akamalizia kwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania Julai 2007 hadi Desemba, 2010. Alichaguliwa na Mkutano wa Viongozi wa Bara la Afrika kuwa Jaji wa Haki za Binadamu na Watu hapo Julai, 2010, na Majaji wenzake walimchagua kuwa Rais wao kwa miaka miwili tokea 2014 hadi 2016, alipo staafu.
Jaji Ramadhani aliwekewa mikono na kuwa padre wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Zanzibar, Desemba, 2013. Mbali na kupata maagizo ya kuandika kitabu hiki, Jaji Ramadhani alimpenda sana Askofu Mkuu Sepeku ambaye aliyagusa maisha yake kwa namna ya kipekee katika viongozi wake wa dini.
Reviews
There are no reviews yet.