Mkuki Na Nyota Publishers

Mkuki na Nyota kushiriki Maonesho ya 32 ya Kimataifa ya Vitabu Tanzania

Dar es Salaam, Tanzania — Ijumaa, 14 Novemba 2025

MAONESHO YA 32 YA KIMATAIFA YA VITABU TANZANIA KUANZIA TAREHE 21–26 NOVEMBA 2025


Mkuki na Nyota Publishers inapenda kuwajulisha wasomaji wote, wadau wa elimu, utamaduni, na tasnia ya uchapishaji kuwa, tutashiriki kikamilifu katika Maonesho ya 32 ya Kimataifa ya Vitabu Tanzania yatakayofanyika kuanzia tarehe 21 hadi 26 Novemba 2025 katika Viwanja vya Maktaba Kuu ya Taifa, Dar es Salaam.

Ushiriki huu unalenga kutoa fursa kwa wasomaji, wazazi, walimu, wadau wa fasihi na elimu pamoja na umma kwa ujumla ili kupata uzoefu wa karibu kuhusu kukuza na kuboresha mazingira ya usomaji kwa kizazi cha leo na kizazi kijacho.

Katika maonesho haya, tutauza na kutangaza vitabu tuvyochapisha; vikiwemo vitabu vya watoto, riwaya, tamthiliya, ushairi, wasifu na tawasifu, sanaa, na historia na rejea. Tutawasilisha ubunifu unaolenga kupanua namna jamii inavyopokea na kufurahia simulizi, fasihi na maarifa kwa kupitia Digidigi, chapa mpya ya Mkuki na Nyota yenye maudhui ya sauti.

Kila simulizi ina nguvu ya kugusa maisha. Pia, inastahili kusimuliwa, kusikika na kuishi. Digidigi ina lengo la kukuza, kuboresha na kuendeleza fasihi. Kupitia jukwaa hili, wasomaji wataweza kufurahia vitabu vya sauti (audiobooks), podcast na maudhui ya sauti yanayowalenga wasikilizaji wa rika zote popote walipo na wakati wowote.

Pia, Mkuki na Nyota itaeleza zaidi kuhusu Kalam Salaam – jukwaa shirikishi la Fasihi ya Kiswahili lililobuniwa kwa kushirikiana na Alliance Française, Dar es Salaam na Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania. Kupitia Kalam Salaam, tumeweza kukuza vipaji vya waandishi chipukizi na wabobezi, kuibua mijadala yenye tija, na kutengeneza mazingira endelevu ya kuthamini Fasihi ya Kiswahili katika matukio yaliyofanyika kila Alhamis ya kwanza ya mwezi.

Katika kudumisha misingi ya kuhamasisha usomaji kwa watoto, kutakuwa na Little Champs­ tukio tunalofanya kwa lengo la kuwalea wasomaji chipukizi wenye umri wa miaka 4–9.  Tukio hili hufanyika kila mwezi ili kuwajengea watoto mazoea ya kusoma kwa kufurahia,kuwa wabunifu na kufanya midahalo ya hadithi, michezo, usanifu wa sanaa na shughuli shirikishi.

Katika kipindi chote cha maonesho, wasomaji watapata na fursa za kukutana na waandishi wa Mkuki na Nyota kwa ajili ya kuzungumza na wasomaji na kusaini vitabu. Baadhi ya waandishi watakaoshiriki ni pamoja na:

  • Balozi Christopher Liundi – Mara Yangu ya Kwanza, Quotable Quote of Mwl. Nyerere
  • Bi. Sauda Simba – Saa Ngapi?
  • Bi Blandina Lucas – Zawadi
  • Ndg. Amri Abdallah – Mtale wa Ngariba
  • Ndg. Shaaban Maulid – Utubora Uzalendo

Ratiba rasmi ya matukio, siku na muda wa mikutano na waandishi itatangazwa kupitia kurasa zetu za mitandao ya kijamii na kwenye banda letu katika eneo la maonesho.

Mkuki na Nyota inawaalika wazazi, walimu, wasomi, wanafunzi, wachapishaji, na wapenzi wa vitabu kutembelea banda letu

Maonesho haya yanaratibiwa na Chama cha Wachapishaji Tanzania (PATA).

Hakuna Kiingilio. Karibuni!

Kwa ajili ya agizo au kupata maelezo zaidi, wasiliana na:
Mkuki na Nyota Publishers
+255 746 088 892
[email protected]
www.mkukinanyota.com

KUHUSU MKUKI NA NYOTA PUBLISHERS
Mkuki na Nyota Publishers ni mchapishaji huru mkubwa zaidi nchini Tanzania. Ilianzishwa mwaka 1980, na kwa zaidi ya miaka 45 imekuwa mstari wa mbele katika kuchapisha sauti za Kiafrika na kuwasilisha mitazamo mbalimbali ya bara hili kwa wasomaji duniani kote.

MNN inajivunia kuchapisha kazi za waandishi mashuhuri wa Afrika, wakiwemo marais watatu wa Tanzania, mshindi wa Tuzo ya Nobel (Abulrazak Gurnah), majaji wakuu wawili wa zamani, na wasomi mashuhuri. Ubora wake umetambuliwa kimataifa kwa tuzo kadhaa zikiwemo: Brittle Paper Publisher of the Year 2024, ASAUK Outstanding African Studies Award, na Best Children’s Book Publisher katika Maonesho ya Vitabu ya Watoto ya Bologna—ikiwa ni mara ya kwanza kwa mchapishaji wa Afrika Mashariki kushinda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *