Dogoli, kijana shababi kutoka kwenye ukoo maarufu anachumbiwa mke na shangazi yake. Mchumba ni Kijakazi. Taratibu zote zinafuatwa na sherehe kubwa ya harusi inaandaliwa. Kama ilivyo katika mila na desturi za watu wa Pwani, harusi haikamiliki hadi jambo moja muhimu sana kutendeka. Kwa mila na desturi hizo, bwana harusi anapaswa kumwingilia bibi harusi kimwili mbele ya somo yake huku wageni wakisubiri kwa hamu na shauku kubwa jibu la tendo hilo. Muda unawadia na Dogoli na Kijakazi wanapewa chumba. Baada ya kuhaha na kuhangaika mle chumbani kwa muda huku jasho likimmiminika kama mchoma mabiwi ya mkaa, ama kutokana na kitete, ama kuwa si riziki, jogoo lake linashindwa kuwika. Dogoli anashindwa kutimiza tendo la ndoa; yaani jogoo linashindwa kupanda mtungi.
Sasa kijana akiwa pale chumbani anatweta kwa marefu na mapana. Baada ya muda auonao kama mwaka mzima, taratibu anachukua nguo zake na kuvaa, mgonjwa, kwa aibu isiyo na kifani. Habari zinatapakaa nje kuwa jogoo la Bwana harusi haliwiki – si matusi, si nyimbo za kejeli, fujo na umbea huku kila mtu akisema lake; yote yalitanda, “Dogoli si riziki; jogoo lake haliwiki, jongoo halipandi mtungi.” Iliyokuwa iwe furaha kubwa kwake na jamaa zake inageuka kuwa huzuni kubwa.
“Ooh! Chaudele wangu, dume langu shababi, baba yangu kuzimu nimekukosea nini? Nimeumbuka mimi jamani; si bure, kuna mkono wa mtu si bure, kuna mkono wa mtu,”
Mama Dogoli amlilia mwanawe kwa uchungu
Katika muendelezo wa kisa hiki cha kusikitisha Dogoli anakufa katika mazingira ya kutatanisha na anazikwa kwa kufuata mila zao. Baada ya maziko wanakijiji wanaamua kuwatuma wajumbe wawili kwenda ughaibuni kwa waganga wa jadi kubaini sababu ya kifo cha Dogoli.
Kuhusu Mwandishi
Athumani Mauya ni mwalimu mstaafu kutoka Bagamoyo. Anaishi Jijini Dar es Salaam na familia yake. Riwaya yake hii ina madhumuni ya kuhifadhi uelewa wa mila za watu wa Pwani kwa manufaa ya vizazi vya leo na vijavyo.
Reviews
There are no reviews yet.