Mkuki na Nyota Publishers kwa fahari kubwa imefanya uzinduzi wa kitabu, Mara Yangu ya Kwanza, kumbukumbu binafsi za Balozi Christopher Liundi, mwanadiplomasia na mtumishi wa umma mstaafu ambaye amehudumia taifa kwa miongo kadhaa.
Uzinduzi huu ulifanyika Jumapili, tarehe 14 Septemba 2025, kuanzia saa 9:00 alasiri hadi saa 12:00 jioni, katika Ukumbi wa Utamaduni wa Urusi (Russian Culture Centre), Jijini Dar es Salaam.
Katika kitabu hiki, Balozi Liundi ameeleza matukio mbalimbali yalivyomtokea kwa mara ya kwanza maishani mwake na katika taaluma yake—kutoka maisha ya utotoni na familia, hadi hatua kubwa za utumishi serikalini na katika diplomasia. Kwa unyenyekevu, ucheshi na tafakuri ya kina, kitabu kinatoa mwanga wa kipekee kwa msomaji juu ya maisha ya mtu aliyeona na kushiriki katika mageuzi ya kihistoria na kisiasa ya Tanzania.
“Maisha yana mfululizo wa matukio mengi yanayotokea kwa mara ya kwanza, mengine madogo, mengine makubwa, na kila moja hubeba somo muhimu la kushirikisha wengine,” alisema Balozi Liundi, “Kitabu hiki ni jaribio langu la kuandika matukio hayo na mafunzo niliyoyapata.”
Uzinduzi huu, uliokuwa wa mwaliko maalum, uliwakutanisha viongozi wa serikali, wasomi, wanahabari na wadau wa utamaduni. Wageni walisisitiza kwamba simulizi binafsi kama hizi ni urithi muhimu kwa taifa, zikitoa nafasi ya kujifunza na kutafakari safari ya Tanzania katika historia yake ya kisiasa na kijamii.
Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:
Mkuki na Nyota Publishers
+255 746 088 892
[email protected]
www.mkukinanyota.com
KUHUSU MKUKI NA NYOTA PUBLISHERS
Mkuki na Nyota Publishers ni mchapishaji huru mkubwa zaidi nchini Tanzania. Ilianzishwa mwaka 1980, na kwa zaidi ya miaka 40 imekuwa mstari wa mbele katika kuchapisha sauti za Kiafrika na kuwasilisha mitazamo mbalimbali ya bara hili kwa wasomaji duniani kote.
MNN inajivunia kuchapisha kazi za waandishi mashuhuri wa Afrika, wakiwemo marais watatu wa Tanzania, mshindi wa Tuzo ya Nobel (Abulrazak Gurnah), majaji wakuu wawili wa zamani, na wasomi mashuhuri. Ubora wake umetambuliwa kimataifa kwa tuzo kadhaa zikiwemo: Brittle Paper Publisher of the Year 2024, ASAUK Outstanding African Studies Award, na Best Children’s Book Publisher katika Maonesho ya Vitabu ya Watoto ya Bologna—ikiwa ni mara ya kwanza kwa mchapishaji wa Afrika Mashariki kushinda.
KUHUSU BALOZI CHRISTOPHER LIUNDI
Balozi Christopher Liundi ni mwanadiplomasia mstaafu na mtumishi wa umma wa Tanzania mwenye uzoefu wa miongo mingi katika serikali, diplomasia na uongozi. Amehudumu katika nafasi mbalimbali za juu serikalini na kuiwakilisha Tanzania kimataifa katika vipindi muhimu vya kihistoria. Kama mwandishi na mtoa kumbukumbu, Balozi Liundi analeta sauti ya kipekee katika uandishi wa maisha ya umma nchini Tanzania, akichanganya matukio binafsi, historia ya kisiasa na kumbukumbu za kitamaduni.
