Tuzo ya Kimataifa ya Kiswahili ya Safal (Safal Kiswahili Prize for African Literature) imezidi kutoa fursa kwa waandishi wa Kiswahili kutoka barani Afrika kung’ara. Mwaka huu, diwani ya ‘Mungu Hadanganywi na Hadithi Nyingine’ iliyoandikwa na Edwin Omindo kutoka Kenya, imeingia fainali ya tuzo hiyo kwa mwaka 2024.
Washindi wa fainali hiyo watatangazwa rasmi katika hafla ya tuzo itakayofanyika tarehe 3 Julai 2025, jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Tuzo ya Safal inadhaminiwa na The Safal Group kupitia Mabati Rolling Mills (MRM), na ilianzishwa mwaka 2014 na Dkt. Lizzy Attree pamoja na Prof. Mukoma wa Ngugi kwa lengo la kukuza na kuenzi fasihi ya Kiafrika, hususan katika lugha za Kiafrika, na kuhimiza tafsiri ya kazi kutoka, kati ya, na kwenda kwenye lugha hizo.
Kwa mwaka 2024, zaidi ya miswada 210 iliwasilishwa na kufanyiwa mapitio na jopo la majaji, na hatimaye kuchaguliwa kazi saba zilizofuzu kuingia fainali.
Miswada iliyochaguliwa kuingia fainali ni pamoja na:
- Mungu Hadanganywi na Hadithi Nyingine – Edwin Omindo (Kenya)
- Nderemo za Mtaa – Joel Hamisi (Tanzania)
- Kitanzi cha Mauti – Mayassa Abdallah Chembea (Tanzania)
- Nyaraka za Wafu – Ali Othman Masoud (Tanzania)
- Waadhi – Mohamed Hamid Haji (Tanzania)
- Bure Ghali – Bashiru Abdallah (Tanzania)
- Laana ya Uovu – Mohamed Idrisa (Tanzania)
Mwalimu Abdilatif Abdalla, ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa tuzo hiyo, alisema:
“Inafurahisha sana kuona kuwa tangu mashindano yaanze mwaka 2015, Safal Prize imeendelea kuvutia idadi kubwa ya washiriki kutoka nchi mbalimbali. Ubora wa miswada pia umeongezeka kila mwaka, jambo ambalo linaendelea kuitajirisha fasihi ya Kiswahili.”
Kwa mwaka huu, jumla ya USD 15,000 zitatolewa kwa waandishi wa miswada bora ambayo haijachapishwa, katika vitengo vya riwaya, ushairi, wasifu, tamthilia, na riwaya za picha (graphic novels).
Kama kawaida, miswada inayoshinda huchapishwa na Mkuki na Nyota Publishers, huku mshindi wa ushairi akitafsiriwa kwa lugha ya Kiingereza na kuchapishwa kupitia Africa Poetry Book Fund.
Kwa mujibu wa Anthony Ng’ang’a, mmoja wa wadhamini wa tuzo hiyo:
“Tuzo hii ni zaidi ya kutambua vipaji vya fasihi – ni alama ya kuendeleza utambulisho wa Mwafrika. Kwa kuunga mkono kazi asilia katika Kiswahili, tunalinda na kuinua lugha inayowaunganisha, kuwahamasisha na kuwawezesha mamilioni ya watu barani Afrika.”
