Dar es Salaam, Tanzania — Jumanne, 22 Julai 2025
Uzinduzi wa Kitabu cha Living with Cancer cha Prof. Mark Mwandosya kufanyika Dar es Salaam
Maisha, maradhi sugu na uongozi wa umma katika simulizi ya kusisimua
Dar es Salaam – Mkuki na Nyota Publishers inayofuraha kutangaza uzinduzi rasmi wa kitabu kipya cha Living with Cancer: Diaries of a Multiple Myeloma Patient, kilichoandikwa na Profesa Mark Mwandosya—msomi mashuhuri, mstaafu wa baraza la mawaziri, na mwanasiasa wa muda mrefu nchini Tanzania.
Uzinduzi huu utafanyika Jumanne, tarehe 29 Julai 2025, kuanzia saa 9:00 alasiri -12:00 jioni, katika hoteli ya Four Points by Sheraton (New Africa Hotel), jijini Dar es Salaam.
Mgeni rasmi katika hafla hii atakuwa Mhe. Doto Biteko, Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia, kutakuwa na mchango kutoka kwa Dkt. Clara Chamba mtaalamu wa magonjwa ya damu na mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), ambaye atatoa mtazamo kuhusu hali ya huduma za saratani nchini, na umuhimu wa utafiti wa kina, uchunguzi wa mapema na huduma jumuishi kwa wagonjwa wote.
Katika simulizi hii ya kipekee, ya wazi na yenye kugusa hisia, Prof. Mwandosya anasimulia safari yake ya kuishi na ugonjwa wa Multiple Myeloma, aina adimu ya saratani ya damu inayodumu kwa muda mrefu. Kupitia maelezo ya ndani na ya binafsi, anashirikisha changamoto na mafunzo ya kimwili, kiakili na kiroho aliyopitia, akisisitiza ujumbe wa matumaini, ujasiri na heshima kwa maisha. Living with Cancer ni zaidi ya kumbukumbu ya binafsi—ni wito wa huruma, uelewa wa umma na huduma zinazomjali mgonjwa.
“Ugunduzi wa saratani haupaswi kuchukuliwa kama hukumu ya kifo,” anaandika Prof. Mwandosya. “Ni safari ya kuendelea kuishi na kutafuta maana na nguvu hata katikati ya maradhi.”
Dibaji ya kitabu hiki imeandikwa na Mhe. Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye amekitambua kama chachu yenye uwezo wa kuhamasisha watu binafsi pamoja na kutoa fikra mpya kwa watunga sera. Akiandika:
“Kitabu hiki kina ujumbe mahsusi kwa watunga sera na watoa huduma za afya [… kinachochea] ari mpya ya kuimarisha juhudi zetu za kukabiliana na changamoto inayokua ya ugonjwa wa saratani; ikiwa ni pamoja na mikakati ya uchunguzi wa mapema na kuhakikisha huduma zote
muhimu za kitabibu zinapatikana nchini.”
Uzinduzi huu ni wa mwaliko maalum tu, na unatarajiwa kuwahusisha wadau wakuu kutoka sekta ya tiba, sera za umma, taaluma, asasi za kiraia na vyombo vya habari—wote wakiwa na dhamira ya pamoja ya kutumia kitabu hiki kama chombo cha uponyaji, utetezi, na mabadiliko ya kimfumo.
Kwa mawasiliano na uthibitisho wa ushiriki, tafadhali wasiliana na:
Mkuki na Nyota Publishers
+255 746 088 892
[email protected]
www.mkukinanyota.com
KUHUSU MKUKI NA NYOTA PUBLISHERS
Mkuki na Nyota Publishers ni mchapishaji huru mkubwa zaidi nchini Tanzania. Ilianzishwa mwaka 1980, na kwa zaidi ya miaka 45 imekuwa mstari wa mbele katika kuchapisha sauti za Kiafrika na kuwasilisha mitazamo mbalimbali ya bara hili kwa wasomaji duniani kote.
MNN inajivunia kuchapisha kazi za waandishi mashuhuri wa Afrika, wakiwemo marais watatu wa Tanzania, mshindi wa Tuzo ya Nobel (Abulrazak Gurnah), majaji wakuu wawili wa zamani, na wasomi mashuhuri. Ubora wake umetambuliwa kimataifa kwa tuzo kadhaa zikiwemo: Brittle Paper Publisher of the Year 2024, ASAUK Outstanding African Studies Award, na Best Children’s Book Publisher katika Maonesho ya Vitabu ya Watoto ya Bologna—ikiwa ni mara ya kwanza kwa mchapishaji wa Afrika Mashariki kushinda.
KUHUSU PROFESA MARK MWANDOSYA
Profesa Mark Mwandosya ni miongoni mwa wataalamu wa sera na wasomi mahiri zaidi waliowahi kulihudumia taifa. Alikuwa Waziri katika wizara mbalimbali zikiwemo za nishati, mazingira na maji, na pia aliwahi kuwa Mbunge wa Rungwe Mashariki (2000-2015). Kimataifa, anatambulika kwa mchango wake katika mazungumzo ya mabadiliko ya tabianchi, maendeleo endelevu, na sera za nishati barani Afrika.
Akiwa na taaluma ya uhandisi na usomi, Prof. Mwandosya alipata Shahada ya Uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza, na amewahi kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Uongozi wake umejenga misingi ya sera kuu katika sayansi, teknolojia na rasilimali za taifa, na anabaki kuwa sauti muhimu katika mijadala ya kitaifa.
